TIMU ya Taifa ya Chad ‘Les Sao’ imejiondoa katika michuano ya kuwania kufuzu kwa Fainali za Mataifa Afrika (AFCON)



TIMU ya Taifa ya Chad ‘Les Sao’ imejiondoa katika michuano ya kuwania kufuzu kwa Fainali za Mataifa Afrika (AFCON) itakayofanyika mwaka 2017 nchini Gabon. Taarifa ya kujitoa kwa Chad ilitolewa na Shirikisho la Mpira wa Miguu barani Afrika (CAF) jana baada ya Les Sao kuandika barua ya kujitoka katika mashindano hayo ikiwa katika kundi G pamoja na timu za Tanzania, Nigeria na Misri.
Chad ilitarajiwa kucheza leo dhidi ya Taifa Stars katika Uwanja wa Taifa Dar es Salaam, ikiwa ni mchezo wa marudiano wa kundi G baada ya kucheza mchezo wa awali jijini N’Djamena katikati ya wiki iliyopita.
Katika mchezo wa awali uliochezwa Uwanja wa Idriss Mahamat Ouya, Taifa Stars iliibuka na ushindi wa bao 1- 0 , bao lililofungwa na nahodha, Mbwana Samatta dakika ya 30 ya mchezo. Kufuatia kujitoa kwa Chad, matokeo ya michezo yote iliyoihusisha timu hiyo yanafutwa, na msimamo wa kundi G kwa sasa unaongozwa na Misri yenye pointi 4, Nigeria pointi 2 na Tanzania pointi 1.
Awali, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, John Magufuli aliitakia heri timu ya Taifa yaTanzania (Taifa Stars) ambayo leo ingecheza na Chad. Kaimu Mkurugenzi wa Mawasiliano, Ikulu, Gerson Msigwa alisema katika taarifa yake ya jana kuwa, Rais Magufuli aliwataka wachezaji, benchi la ufundi na viongozi wa TFF kutambua kuwa Watanzania wana matumaini makubwa kuwa timu yao itafanya vizuri katika mchezo huo.
Endapo Stars ingecheza na kushinda leo basi ingefikisha pointi saba na kuipita Nigeria na kama ingeshinda kwa mabao mengi, ingeweza kushikilia kwa muda uongozi wa kundi hilo. Hata hivyo kujitoa kwa Chadi kumekuwa pigo kwa Stars kwa kuwa sasa inabaki kuwa ya tatu.
Awali msemaji wa TFF, Baraka Kizuguto alisema hawakuwa na taarifa zozote za kuwasili kwa Chad na wala hawakuwa na taarifa kama timu hiyo imeshindwa kuja nchini kutokana na ukata kama baadhi ya watu walivyodai.
“Hadi sasa hatuna taarifa zao na hatujapata taarifa kama Chad wamejitoa kwa sababu ya ukata, ebu muulize vizuri aliyekupa taarifa hizo, “alisema Kizuguto jana mchana. Licha ya Chad, kujitoa lakini kocha wa Stars Boniface Mkwasa, alisema kikosi chake kilikuwa tayari kwa ajili ya mchezo huo wa leo na lengo lao kubwa ni kuendeleza ushindi walioupata ugenini Chad Jumatano iliyopita.
Kocha huyo alisema awali walikuwa na majeruhi wawili beki Kelvin Yondani na kiungo Mwinyi Kazimoto, lakini juzi walianza mazoezi hivyo angewatumia sambamba na mshambuliaji Abdillah Yusuf, aliyejiunga kwa mara ya kwanza na timu hiyo akitokea klabu ya daraja la pili ya Mansfield ya England. Rais wa TFF, Jamal Malinzi alikuwa amemtangaza Waziri Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania Kassim Majaliwa kuwa mgeni rasmi katika pambano hilo .
by Epiphan Bernardi

No comments:

Post a Comment