WIKI iliyopita, Dk Mohamed Shein, aliapishwa rasmi kuiongoza Zanzibar katika kipindi kingine cha miaka mitano.

WIKI iliyopita, Dk Mohamed Shein, aliapishwa rasmi kuiongoza Zanzibar katika kipindi kingine cha miaka mitano. Wakati Dk Shein anaapa na kujipanga kuanza ngwe nyingine ya uongozi wa visiwa hivyo, upande wa pili wa shilingi, Chama cha Wananchi (CUF) ambacho kwa miongo kadhaa kimekuwa sehemu ya siasa za Zanzibar, kilikaririwa kikisema kwamba hakimtambui Shein na hakiko tayari kufanya naye kazi
katibu mkuu wa CUF Maali m Seif Sharif Hammad

Kinachoonekana ni kwamba, ingawa matokeo ya urais wa Zanzibar ya Oktoba 25 hayajawahi kutangazwa hadharani na chombo husika ambacho ni Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), CUF inaamini kwamba aliyekuwa mgombea wao wa urais, Maalim Seif Sharif Hamad alishinda uchaguzi huo.Kilichoifikisha CUF hapo ni madai ya kutotambua uchaguzi wa marudio uliofanyika Machi 20 huku kikisisitiza kwamba uchaguzi huo wa marudio ulikuwa batili. Chenyewe kinataka matokeo yatakayotangazwa yawe yale ya uchaguzi uliofutwa, uliofanyika Oktoba 25 mwaka jana.
Kinachonishangaza kuhusu imani hiyo ambayo nimegundua kwamba wapo Watanzania wanayoiamini ikiwa ni pamoja na baadhi ya nchi za nje, ni tangazo lilitolewa na Maalim Seif mwenyewe kwamba ameshinda uchaguzi. Inaelezwa kwamba Maalim Seif alijitangazia ushindi asubuhi ya Oktoba 26, yaani siku moja tu baada ya kupiga kura, kinyume na taratibu.
Katika video moja inayosambazwa kwenye mitandao ikimuonesha Maalim Seif akijitangazia matokeo, anasema alipata kura 277,000 sawa na asilimia 52.87 na kwamba mgombea wa CCM, alipata kura 178,363 sawa na asilimia 47.13. Ukijumlisha hizo asilimia utaona ni asilimia 100 sawa na kura 455,363. Kwa mantiki hiyo tangazo hilo halioneshi kura zilizoharibika wala walizopata wagobea urais wengine katika uchaguzi uliokuwa na wagombea urais 14.
Hilo pekee linaacha maswali kuliko majibu. Lakini nimekuwa ninajiuliza, ingekuwaje kama vyama vingine navyo vingejitangazia ushindi, tuseme CCM ikasema imepata asilimia 60, chama cha Alliance for Democratic Change (ADC) nacho kikaibuka kutangaza kimeshinda kwa asilimia 54, na kingine na kingine ingekuwaje? Lakini hayo tuyaache. Tuchukulie kwamba CUF ilishinda au ingelishinda kama uchaguzi usingefutwa kwa sababu za matatizo yaliyojitokeza ambayo yalitangazwa na tume.
Matatizo hayo ni pamoja na makamishna wa uchaguzi katika ZEC kupigana kutokana na tofauti zao, makamishna kuonesha upendeleo na baadhi ya vituo, hususan kisiwani Pemba kura zilizopigwa kuonekana ni zaidi ya zilizosajiliwa.
Mengine ni masanduku ya kupigia kura kutopewa ulinzi wa kutosha na mawakala pamoja na maafisa wa uchaguzi, mawakala wa vyama kufukuzwa katika vituo kadhaa, watu kuvamia vituo vya kupigia kura kwa lengo la kuzua ghasia, vyama vya kisiasa kuingilia tume mara kwa mara na kura kuharibiwa hususan zile za Pemba. Kama kuna kasoro hizo zinatakiwa na CUF inaamini ilishinda kihalali, hakukuwa na haja ya kuwa na hofu kurudia uchaguzi kwani ingeshinda tena.
Je, ilihofu nini? Inawezekana ilikuwa haiiamini Tume ingawa nayo ina wajunbe wake, lakini nimekuwa ninajiuliza kwa nini ilikataa moja kwa moja marudio ya uchaguzi badala ya kuweka masharti kuhusu kuiboresha Tume? Mimi ningeungana na CUF kama wangekubali kurudia uchaguzi, halafu wakataka masharti fulani yatimizwe kwa njia ya mazungumzo kama vile kufumua upya ZEC na mengine kama hayo ambayo kila mtu akiyasikia yanamuingia akilini.
Ninasema hivyo kwani bado ninaamini kwamba katika mazingira ambayo chama chochote nacho kingeweza kuibuka na kudai kuwa ndicho kilichoshinda, ni uchaguzi wa marudio tu ndilo lilikuwa suluhisho. Kama CUF wangekuja na mapendekezo kuhusu namna ya kufanya tume ionekane ni huru zaidi, mapendekezo ambayo kila anayeyasikia anaona yangesababisha uchaguzi huru na kupatikana mshindi bila upendeleo, halafu mapendekezo hayo yakapingwa na watawala katika uchaguzi wa marudio, mimi ningekuwa upande wa CUF.
Kusema tu kwamba Mwenyekiti wa Tume ya Uchaguzi ya Zanzibar (ZEC), Jecha Salim Jecha hakuwa na uhalali wa kisheria kufuta uchaguzi, kung’ang’ana kwamba uchaguzi uliofutwa haukuwa na kasoro bila kukiri kwamba kujitangazia matokeo lilikuwa kosa pia na hivyo kuona umuhimu wa kurudia uchaguzi katika mazingira yaliyoboreshwa zaidi, mimi sioni kama CUF walitenda haki kwa Wazanzibari na wao pia kujitendea haki.
Ni kwa mantiki hiyo, ningeishauri CUF kukaa chini na kukiri upungufu na kisha kuungana na serikali iliyotawazwa majuzi katika kuijenga Zanzibar na kuacha kile vijana siku hizi wanaita ‘figisufigisu’. Hii ni kwa sababu hakuna namna nyingine ya kupambana na serikali ya Shein isipokuwa kuidhoofisha ili ishindwe kutekeleza majukumu yake na hili halitawaathiri viongozi kama Seif wanaoweza kutibiwa India na kuishi kwa siku kadhaa kwenye hoteli za kitalii kama Serena, bali wananchi wa kawaida wa visiwa hivyo.
Upinzani na demokrasia ya ndani Katika muktadha huo huo, ninapenda kutumia fursa hii kuvitaka vyama vya upinzani kuzingatia pia kila wakati demokrasia ndani ya vyama vyao kuliko kuangalia ya nje zaidi huku vikipuuza ya ndani. Imani yangu ni kwamba vyama vya upinzani vinapokuwa vinaimarisha demokrasia ya ndani, vitapata watu wengi wa kuviunga mkono kuliko vinaporuka kipengele hicho na kulalamika pale vinaposhiriki chaguzi na kuhisi kama demokrasia inaminywa na walioko madarakani.
Sisemi kwamba naunga mkono demokrasia kuminywa kwa aina yoyote ile, lakini nimekuwa nikikatishwa sana tamaa na upinzani linapokuja suala la demokrasia ya ndani. Labda nitoe mfano hai. Katika kumpata mgombea wake wa urais wa Jamhuri, Chama Cha Mapinduzi kilionesha demokrasia pana zaidi kwa kuruhusu wanachama wake wengi kujitokeza kugombea na kisha kujadiliwa na vikao husika kabla ya kupitishwa.
Vikao hivyo ni kuanzia kamati kuu, halmashauri hadi mkuano mkuu wa chama hicho. Hata kukata baadhi ya majina yaliyoonekana hayakidhi vigezo vilivyoweka na chama hicho, lakini mtu ungeweza kuona namna demokrasia ilivyochukua mkondo wake ndani ya CCM hadi akapatikana mgombea, John Magufuli. Lakini mgombea aliyewakilisha muungano wa upinzani (Ukawa) kwa urais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania alipatikana ‘kidikteta’.
Uwanja mpana haukutolewa ili mgombea huyo apambane na watu wengine waliokuwa na nia ya kugombea urais kupitia Ukawa. Tulichoona ni baadhi ya watu kama Profesa Ibrahim Lipumba aliyekuwa ameshapitishwa na CUF ili kupambana na wagombea wengine ambao wangeteuliwa na vyama vingine vilivyokuwa vinaunda Ukawa, akiamua kubwaga manyanga.
Hali hiyo ya kutoruhusu demokrasia kuchanua ndani ya vyama vya upinzani na uroho wa madaraka ndio chanzo cha kuanzishwa kwa vyama kama ACT - Wazalendo, hali inayopunguza nguvu za upinzani. Tukija kwa CUF, kumbukumbu zinaonesha kwamba mazingira yalikuwa yale yale ya miaka nenda miaka rudi. Sisemi kwamba haikuwa halali Maalim Seif kugombea lakini alipambanishwa na akina nani?
Sana sana kumbukumbu zilizopo ni za watu kama Hamad Rashid Mohamed kutimuliwa na kisha kubwaga manyanga na kukimbilia ADC baada ya kuonekana naye anautaka ‘Umaalim Seif’! Mtu anaweza kujiuliza hoja hii imekujaje kwenye makala haya, lakini majibu ni kama nilivyogusia hapo juu, ni kama wanavyosema wahenga kwamba ukarimu lazima uanzie nyumbani.
Upinzani ungeimarika zaidi na kuungwa mkono kila wakati kama wenyewe ungekuwa unaendesha demokrasia ya uhakika ndani na hivyo unapolalamikia demokrasia nje unakuwa na uhalali wa asilimia 100.
by Epiphan Bernardi

No comments:

Post a Comment