Tume ya taifa ya uchaguzi nchini Kenya, IEBC, imetangaza kwamba robo ya vituo vyote vya kupigia kura nchini humo havina huduma nzuri ya mtandao wa simu wa 3G au ya 4G.

Robo ya vituo vyote vya kupigia kura nchini Kenya havina huduma nzuri ya mtandao wa simu wa 3G na ya 4G.  



Tume ya taifa ya uchaguzi nchini Kenya, IEBC, imetangaza kwamba robo ya vituo vyote vya kupigia kura nchini humo havina huduma nzuri ya mtandao wa simu wa 3G au ya 4G.
Tume hiyo imesema maafisa wasimamizi wa uchaguzi katika vituo hivyo watalazimika kusongea hadi maeneo yenye huduma nzuri ya mtandao ndipo waweze kupeperusha matokeo.
Uchaguzi mkuu nchini Kenya utafanyika Jumanne tarehe 8 Agosti.
Taarifa ya tume hiyo inasema kuna jumla ya vituo 11,155 ambavyo havina huduma nzuri ya mtandao ya 3G kati ya jumla ya vituo 40,883 kote nchini humo.

"Maafisa wasimamizi wa uchaguzi watatafuta pahala penye huduma nzuri ya mtandao au watumie simu za setilaiti kupeperusha matokeo," tume hiyo imeandika kwenye Twitter.
Vituo hivyo visivyo na huduma nzuri ya simu vinapatikana katika kaunti 45 kote nchini humo.
Ni kaunti za Nairobi na Mombasa pekee ambazo hazijakumbwa na tatizo hilo.
Takwimu kutoka kwa Mamlaka ya Mawasiliano Kenya zinaonesha maeneo mengi nje ya miji nchini humo hayana huduma ya 3G.

Ripoti kuhusu huduma ya simu na mtandao nchini Kenya ya mwaka jana inaonesha huduma ya 3G inapatikana katika asilimia 17 pekee ya ardhi ya Kenya. Hata hivyo, tofauti katika wingi wa watu maeneo mbalimbali, huduma hiyo huweza kufikia asilimia 78 ya wananchi nchini humo.
Ripoti hiyo iliyotolewa na Mamlaka ya Mawasiliano Kenya inasema kufikia wakati huo, kaunti ya Isiolo ndiyo pekee ambayo haikuwa na eneo hata moja ambalo lina huduma ya 3G.
Katika maeneo mengi, huduma inayopatikana ni ya 2G.
Hayo yakijiri, afisa mkuu mtendaji wa IEBC Ezra Chiloba pia amefafanua kwamba karatasi za kupigia kura zitahitajika kuwa na muhuri wa tume hiyo kabla ya mpiga kura kupiga kura.
Amesema karatasi ambazo zitapatikana ndani ya masanduku ya kura zikiwa hazina muhuri hazitahesabiwa kama kura halali.
Marekebisho katika kanuni na sheria za uchaguzi yaliyofanywa mwaka huu yalikuwa yamefutilia mbali hitaji la kuwepo kwa muhuri katika karatasi za kura.
Hata hivyo, Bw Chiloba amesema tume hiyo imeamua kuwa karatasi za kura ni lazima zipigwe muhuri.

No comments:

Post a Comment